UNAZIJUA FAIDA HIZI 9 ZA CHUNGWA?

NI msimu mwingine wa machungwa, yamejaa tele kila kona. Shilingi 100 tu unapata chungwa. Lakini siyo ajabu kama kuna watu msimu unaisha hawajala hata chungwa moja, wala suala la matunda halipo kabisa katika orodha ya milo yao! Inawezekana pia hata kwa wale wanaokula, japo kidogo, hula kama kiburudisho tu bila kujua faida zake mwilini. Katika makala ya leo nitakujuza faida 9 unazoweza kuzipata unapokula chungwa, ambalo limesheheni virutubisho kibao. Kumbuka kuwa hata chungwa moja tu ukila linakidhi yale mahitaji muhimu ya mwili ya kila siku (daily requirement), iwe chungwa lenyewe au juisi yake halisi. 1.UKOSEFU WA CHOO Kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha kirutubisho aina ya kambalishe (fibre), chungwa husaidia usagaji wa chakula tumbuni na hutoa ahueni kwa mtu mwenye matatizo ya ukosefu wa choo. Aidha, kambalishe huondoa kolestro na huimarisha kiwango cha sukari mwilini, hivyo chungwa ni zuri kwa wagonjwa wa kisukari. 2.UGONJWA WA MOYO Kiwango kikubwa cha Vitamin C na virutubisho vya ‘flavonoids’, ‘phytonutrients’ vilivyomo kwenye chungwa, huondoa kwa mlaji hatari ya kupatwa na magonjwa ya moyo (Cardiovascular disease)! 3. SHINIKIZO LA DAMU Virutubisho vya Magnesi (Magnesium) na ‘hesperidin’ vilivyomo kwenye chungwa, husaidia kuondoa tatizo la shinikizo la damu la juu (high blood pressure), hivyo machungwa ni mazuri kwa wagonjwa wa presha. 4. MIFUPA NA MENO Chungwa lina kiasi kingi cha madini ya kalisi (calcium) ambayo ni muhimu kwa uimarishaji wa mifupa na meno. 5. KOLESTRO Virutubisho vilivyomo kwenye chungwa, hasa kwenye maganda yake, hupunguza kiwango cha mafuta mabaya mwilini (bad cholesterol). Hivyo kwa wenye tatizo la lehemu wanashauriwa kula machungwa pamoja na nyama zake. 6. KINGA YA MWILI Vitamin C iliyomo kwenye chungwa huimarisha uzalishaji wa seli nyeupe ambazo ni muhimu kwa uimarishaji wa kinga ya mwili. Unapokuwa na kinga imara, huwezi kusumbuliwa na magonjwa mara kwa mara, yakiwemo malaria. 7. VIDONDA VYA TUMBO Unapokuwa na kiwango cha kutosha cha Vitamin C mwilini, una uhakika na kinga dhidi ya ugonjwa wa vidonda vya tumbo, na kama tayari unavyo, ulaji wa machungwa utakupa ahueni. 8. UGONJWA WA MAFUA Kutokana na wingi wa virutubisho vya kinga vilivyomo kwenye chungwa, ulaji wake mara kwa mara utakuepusha na magonjwa ya kuambukiza na vairasi (virus), kama vile mafua ambayo hivi sasa yanawasumbua watu wengi. Hivyo kula machungwa mengi kadri uwezavyo ili ujiepushe na mafua kwa sasa. 9. KINGA YA MAGONJWA MENGI Chungwa, siyo tu linatoa kinga kwa magonjwa yaliyoainishwa hapo juu, bali pia hutoa kinga hata kwa magonjwa mengine kama vile baridi yabisi (arthritis, rheumatism), pumu, kikohoo, kifua kikuu, nimonia na kisukari. Nakushauri kula machungwa au juisi yake halisi kuanzia leo ili kupata faida hizo.

Ahsante sana Global publishers

TUPE MAONI YAKO
 

SULEIMAN MAGOMA Copyright © 2011 -- Template created by Suleiman Magoma -- Powered by Magoma Co.LTD